Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone.
Na Nathaniel Limu, Singida
MKUU wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, amezitaka halmashauri za wilaya na manispaa, kuweka mipango endelevu ya kuongeza michango ya wananchama wa mifuko ya afya ya jamii (CHF) na TIKA, ili mkoa uweze kujijengea uwezo wa kutoa huduma bora kwa wanachama wa mifuko hiyo.
Dk. Kone ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha kazi cha kuhamasisha CHF na TIKA kwa viongozi wa mkoa na halmashauri zote mkoani hapa.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan,alisema ingawa mkoa wa Singida unafanya vizuri katika uendeshaji wa mifuko hiyo,hata hivyo idadi ya wanachama hai waliojiunga na mifuko hiyo,bado ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya wananchi ambao hawajajiunga.
“Naagiza kila halmashauri iweke bajeti kwa ajili ya zoezi la uhamasishaji kwa wananchi,ili waweze kuielewa vizuri mifuko hii na faida zake”, alisema Dk.Kone na kuongeza kwa kusema;
“Tufanye hivyo kwa ustadi mkubwa na kusisite kuwashirikisha pia wadau wetu muhimu wa mfuko huu,ndugu zetu wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF)”.
Awali kaimu meneja wa NHIF mkoa wa Singida, Salum Adamu, alisema lengo la kikao hicho cha uhamasishaji wa mifuko ya CHF na TIKA,ni kuwajengea uwezo zaidi viongozi wa mkoa na wa halmashauri za wilaya na manispaa ili shughuli ya uhamasishaji iweze kuwa na tija zaidi.
Katika hatua nyingine,Adamu alisema dhana ya mipango ya bima za afya ulimwenguni kote,ni kutengeneza ushirikianao/fungamano la wanachama ambao kwa pamoja hupata kinga dhidi ya gharama za tiba pindi wanapougua na kuhitaji tiba.
“Fungamano hili lina misingi ya ushirikiano wa kindugu na kibinadamu dhidi ya gharama za tiba.Haina misingi ya kibiashara wala lengo la kutengeneza faida kwa namna yo yote ile”,alifafanua kaimu meneja huyo.
Kuhusu matarajio ya bima ya afya,Adamu alisema mufuko huo wa CHF na NHIF,imeboreshwa na inaendelea kuboreshwa zaidi kuhusiana na kitita cha mafao kwa kadri ya uwezo wa mifuko itakavyoruhusu.
“Mifuko yetu tutaendekea kuimarisha katika utoaji wa elimu kwa wadau juu ya haki na wajibu wao,tutaendelea kuboresha huduma kwa kutoa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa vituo na tutaendelea kuimarisha CHF ili kuwezesha Watanzania wengi na hasa wa vijijini kuwa na mapango madhubuti wa matibabu”,alisema Adamu kwa kujiamini.